Zaidi ya bilioni 46 kukarabati uwanja wa ndege kigoma
22 April 2024, 15:24
Katika kuhakikisha sekta ya usafirishaji nchini inaimarika serikali imeendelea kufanya maboresho na kukarabati viwanja vya ndege ikiwemo kiwanja cha ndege kigoma ili kurahisha urafirishaji.
Na Lucas Hoha – Kigoma
Zaidi ya shilingi Bilioni 46 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la abiria, sehemu ya maegesho ya ndege zaidi ya sita kwa wakati mmoja na kujenga jengo la waongoza ndege katika uwanja wa ndege Kigoma uliopo Manispaa ya Kigoma Ujiji utakaotekelezwa ndani ya miezi 18, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya serikali kuufungua mkoa wa Kigoma kibiashara kitaifa na kimataifa.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa miradi ya viwanja vya ndege Tanzania mhandisi Neema Mwasha mara baada ya ziara fupi iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa viwanja vya ndege.
Mwasha amesema mradi huo utakuwa na manufaa kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma kwani uwanja huo utapokea ndege kutoka mataifa tofauti hatua itakayochochea maendeleo.
Kwa upande wake, Mhandisi wa mradi huo kutoka kampuni ya China Railway Construction Engineering Group ambao ndio wamepewa tenda ya ujenzi wa mradi huo Emmanuel Lubanza, amesema mpaka sasa wamefikia asilimia 4.7 ya ujenzi na kuwa wamechelewa kutekeleza mradi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha hivyo mvua zikapopungua watafanya kazi usiku na mchana ili kuendana na mkataba.
Nao baadhi ya wadau wengine walioshiriki kwenye ziara hiyo akiwemo Balozi wa ubalozi mdogo wa Burundi Mkoani Kigoma nchini Tanzania Kekenwa Jeremie amesema uwanja huo utakuwa na manufaa kwa wananchi wa nchi jirani kwani watautumia katika kufanya biashara.
Masuala mengine ambayo wadau wameshauri mara baada ya ziara hiyo ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma wamesema serikali haina budi kuboresha miundombinu ya barabara za mkoa wa Kigoma.