Madiwani Kibondo wasisitiza upatikanaji wa dawa muhimu
12 March 2024, 13:24
Madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma wameitaka idara ya afya wilayani humo kuhakikisha dawa muhimu zinapatikana muda wote katika zahanati, vituo vya afya na hospitali ya wilaya ili kuondoa usumbufu kwa wagonjwa hasa wajawazito, watoto na wazee.
Akizungumza katika Baraza la Madiwani la halmashauri ya wilaya ya Kibondo, diwani wa kata ya Bitale Bw. Gerevazi Mpagaze amesema kuwa wagonjwa wamekuwa wakipata wakati mgumu kwa kukosa dawa muhimu wakati idara ya afya inapaswa kuhakikisha dawa zinapatikana muda wote.
Amesema kuwa amekuwa akipokea changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi hasa kuhusu huduma za afya huku walio wengi wakilalamikia kukosa dawa na kuambiwa wakanunue kwenye duka la dawa suala ambalo si sawa.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo Dr. Gabriel Chitupila amesema kuwa malengo ya serikali ni kuhakikisha wagonjwa wote hasa wanaopata huduma kupitia bima za afya wanapata huduma muhimu na kwa wakati mwafaka.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo Habili Maseke amewataka waganga wafawidhi katika zahanati na vituo vya afya kutoa takwimu sahihi katika maeneo yao ili bohari ya dawa MSD waweze kufanya kazi yao kwa kuzingatia upungufu uliopo