Watumishi wa umma fuateni maadili ya kazi
8 March 2024, 09:42
Miradi ya maendeleo haiwezi kuwa na viwango kama viongozi hawana maadili ya kazi na viapo vyao.
Na James Jovin.
Watumishi wa umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma wametakiwa kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya kazi na kuwajibika kwa pamoja katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuzuia mianya ya rushwa na kutekeleza miradi chini ya kiwango hali inayoweza kurudisha nyuma maendeleo.
Ushauri huo umetolewa na katibu msaidizi ofisi ya Rais sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kanda ya magharibi Bi. Anna Mbasha akizunguma na waandishi wa habari mara baada y kutoa elimu kwa viongozi wa umma wilayani kibondo kuhusu uwajibikaji wa pamoja na maadili ya kazi.
Aidha bi. Anna amesema kuwa viongozi wa umma wanapaswa kuwajibika kwa pamoja na kuweka mpango mkakati wa shughuli za serikali kwa pamoja ili kufanikisha miradi ya maendeleo na kutokomeza ubadhilifu wa mali ya umma.
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Kumsenga Bw. Radbod Rock ambaye alihudhulia mafunzo hayo ya maadili kwa viongozi wa umma amewataka viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji kutekeleza shughuli zao kwa kufuata miongozo ya serikali.