Serikali yakamilisha ujenzi wa zahanati Busunzu Kibondo
4 March 2024, 12:07
Serikali imesema itaendelea kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha wanaweka miundombinu bora ya vifaa tiba.
Na, James Jovin
Wananchi wa kijiji cha Nyaruranga kata ya Busunzu wilayani Kibondo mkoani Kigoma wameepukana na adha ya kutembea zaidi ya kilometa 20 kutafuta huduma za afya baada ya Serikali kukamilisha zahanati iliyogharimu zaidi ya shilingi milioni mia moja kijijini humo.
Hayo yamebainishwa na Mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Kibondo Dr. Henry Chinyuka wakati wa uzinduzi wa zahanati hiyo itakayosaidia zaidi ya wakazi elfu tano wanaoishi katika kijiji hicho na maeneo jirani.
Aidha Dr. Chinyuka amesema kuwa serikali inaendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga zahanti katika vijiji lakini pia vituo vya afya katika kata ikiwa ni mikakati ya kuhakikisha huduma za afya zinakuwa karibu na jamii na kupunguza vifo hasa akina mama, watoto na wazee.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Muhambwe Dr. Florence Samizi akizindua zahanati hiyo amewapongeza wananchi wa kijiji cha Nyaruranga kwa kujitolea mchango wa zaidi ya shilingi milioni kumi kuanzisha zahanati hiyo na badae serikali kuongeza milioni 67 zilizosaidia kukamilika kwa zahanati hiyo.
Zaidi ya bilioni 9 zimetumika kujenga vituo vya afya, zahanati na kuboresha miundo mbinu katika hospitali ya wilaya ya Kibondo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ikiwa ni mikakati ya serikali katika kuboresha huduma za afya na kusogeza huduma hizo hasa kwa wananchi waishio vijijini.