Bilioni 52 zatekeleza miradi ya maendeleo kibondo
27 February 2024, 16:47
Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma imetekeleza miradi ya zaidi ya shilingi bilioni 52 na kuleta manufaa kwa wananchi.
Na, James Jovin
Zaidi ya shilingi bilioni 52 zimetumika kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo katika wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa barabara za mitaa, uchimbaji wa visima vya maji na uboreshaji wa huduma za afya
Hayo yamebainishwa na mbunge wa jimbo la Muhambwe Dr. Florence Samizi wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kumukugwa katika ziara yake inayoendelea katika vijiji mbali mbali wilayani Kibondo.
Aidha amesema kuwa madaraja ya mawe yapatayo 17 yamejengwa katika barabara mbali mbali hasa za vijijini hali ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa wakulima kupitisha mazao yao lakini pia wanafunzi ambao walikuwa wakilazimika kupita ndani ya maji hasa wakati wa kwenda shule.
Katika hatua nyingine amesema kuwa mikakati ya serikali ni kuhakikisha vijiji vyote vinavyounda wilaya ya Kibondo vinapata umeme ili kuwasaidia wananchi kurahisisha shughuli zao hasa zile zinazohitaji nishati ya umeme na kwamba swala hilo litasaidia sana kuongeza maendeleo miongoni mwa jamii.