Wananchi watakiwa kushiriki mapambano dhidi ya malaria Kibondo
23 February 2024, 12:16
Wananchi wilayani Kibondo mkoani Kigoma kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria ambao umekuwa ukisababisha vifo kwenye jamii.
Na, James Jovin.
Shirika lisilo la kiserikali SADERA kwa kushirikiana na serikali limefanya ziara katika vijiji kumi wilayani Kibondo mkoani Kigoma lengo kubwa ikiwa ni kutoa elimu ya kupambana na ugonjwa wa malaria na matumizi bora ya chandarua kwa wananchi hasa waishio vijijini.
Gerald Nkona ni mratibu wa shirika la SADERA akiwa katika moja ya vijiji vilivyotembelewa kwa lengo la kuelimisha wananchi katika mapambano ya kutokomeza ugonjwa wa malaria amewataka kushiriki ipasavyo ili kuokoa maisha ya akina mama wajawazito, watoto na wazee ambao hufariki kila mara kwa ugonjwa wa malaria.
Aidha amesema kuwa serikali imelenga ifikapo 2030 malaria iwe imetokomezwa kabisa hivyo jamii inapaswa kushiriki ipasavyo katika mikakati hiyo ili ugonjwa huo ubaki kuwa historia kama ilivyo kwa ugonjwa wa ukoma.
Kwa upande wake mratibu wa malaria wilayani Kibondo Dr. Joshua Donasiano amesema kuwa ugonjwa wa malaria bado ni tishio katika wilaya ya Kibondo kutokana na takwimu kuonesha kuwa zaidi ya asilimia 48.7 ya wagonjwa wanaopimwa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali ya wilaya hukutwa na ugonjwa huo.
Malaria, ni ugonjwa ambao bado unaendelea kutishia maisha ya nusu ya watu ulimwenguni kote. Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya ulimwenguni WHO, bara la Afrika ndio linaloongoza kwa visa vya malaria kwa asilimia 90, hususan kusini mwa jangwa la Sahara ambalo linabeba mzigo mkubwa wa ugonjwa huo.
Takwimu za shirika hilo zinaonyesha kuwa mwaka 2021 pekee watu 619,000 walipoteza maisha kutokana na malaria huku wagonjwa wapya wakifikia milioni 247 na asilimia 95 ya vifo na wagonjwa walikuwa katika Ukanda wa Afrika.