Mpango wa msindikizaji unavyopunguza vifo vya mama na mtoto
10 January 2024, 19:28
Wananchi wa halmashauri ya mji Kasulu mkoani Kigoma, wamesifu huduma ya msindikizaji mama mjamzito katika vituo vya afya kuwa imesaidia kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto vinavyotokea wakati wa kujifungua.
Wakizungumza katika kituo cha afya Kiganamo kilichoko halmashauri ya Mji Kasulu, baadhi ya wakazi hao wamesema huduma za usindikizaji mjamzito imechangia pakubwa kuhamasisha wanaume katika jamii kushiriki katika mpango wa serikali wa kuboresha huduma na kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi.
Ibrahimu George ni mkazi wa Kata ya Murusi ambaye ni Baba wa watoto wawili na baadhi ya wananchi wengine hapa wanazungumzia faida za huduma ya msindikizaji.
Akizungumzia huduma ya usindikizaji katika kituo cha afya Kiganamo Halmashauri ya mjini Kasulu, Muuguzi Mkunga ambaye pia ni Mratibu wa Huduma ya Msindikizaji, Tecla Masanja, amesema mpango huo umekuwa na matokeo mazuri.
Afisa Uhamasishaji Jamii kutoka Shirika la Thamini Uhai Ignus Kalongola, amesema mpango huo ambao kwa sasa unatekelezwa katika vituo 15 vya afya na hospitali za wilaya mkoani Kigoma, umesaidia kuongeza idadi ya akina mama wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya afya na kupunguza uwezekano wa kutokea vifo vya uzazi.
Tangu mpango huo uanze mkoani Kigoma miaka sita iliyopita umetajwa kuwa na mafanikio makubwa na unaweza kuishawishi serikali kuona umuhimu wake na kuufanya kuwa mpango wa nchi nzima.