Kibondo na mkakati wa kuongoza kwa usafi wa mazingira kitaifa
3 January 2024, 14:11
Halmashauri ya wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma imeanzisha mkakati wa kuhakikisha usafi wa mazingira unaimarishwa ili kujiweka katika nafasi nzuri za ushindani wa usafi wa mazingira kitaifa hali itakayosaidia kuepuka magonjwa yatokanayo na uchafu ikiwemo kipindu pindu.
Hayo yamebainishwa na afisa afya na usafi wa mazingira wilayani Kibondo Bw. Steven Janks wakati wa kikao kazi kilichofanyika ofisi za Mkurugenzi mtendaji na kwamba lengo ni kushinda mashindano ya kitaifa yanayohusu usafi wa mazingira ambayo hufanyika karibu kila mwaka.
Aidha amesema kuwa wilaya ya Kibondo kupitia kijiji cha Kigendeka mwaka 2013 ilishika nafasi ya tatu katika usafi wa mazingira hali ambayo inatia hamasa kuendelea kufanya vizuri zaidi na hivyo kusaidia kupunguza magonjwa yatokanayo na uchafu na hivyo kuiweka jamii katika hali ya usafi na afya nzuri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo Bw. Habili maseke amewataka viongozi wa kata na vijiji kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi juu ya swala la usafi wa mazingira lakini pia kupitisha sheria ndogo za tozo na faini kwa wale wanaokiuka maelekezo huku wakifuata maelekezo ya mkurugenzi kikamilifu kwa faida ya jamii na serikali kwa ujumla.