Watoto wa miaka mitano hadi 14 kupatiwa dawa za minyoo na kichocho kigoma
22 November 2023, 10:17
Imeelezwa kuwa jamii kushindwa kuzingatia usafi na kuwa na vyoo bora ni miongoni mwa sababu zinazosababisha kuendelea kusumbuliwa na magonjwa ya minyoo na kichocho.
Na Tryphone Odace
Jumla ya Watoto laki tano na tano elfu mia nane na arobaini wenye umri wa miaka mitano hadi kumi na nne wanatarajiwa kupatiwa dawa za minyo na kichocho katika Halmashauri zote za Mkoa wa Kigoma.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Bw. Albert Msovela wakati akingumza na waandishi wa habari juu ya kampeni hiyo ya utoaji wa dawa hizo ambapo amesema tayari maandalizi yamekamilika na lengo ni kutokomeza magonjwa ya minyo na kichocho ambayo yamekuwa yakisumbua watoto.
Naye Mratibu wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele Mkoa wa Kigoma Inocent Msikali amesema ukosefu wa vyoo bora kwenye jamii ya Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa sababu zinazosababisha uwepo wa magonjwa ya minyoo na kichoho kutokana na wengi wao kujisaidia vichakana.
Kwa upande wake, Mwakilishi Kutoka Wizara ya Afya Nashiri Abdallah amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha magonjwa yasiyopewa kipaumbele yanadhibitiwa ili yasiweze kuleta madhara makubwa kwa wananchi.
Wizara ya afya kupitia Mpango wa taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wananchi wanapata kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza ambapo kwa mkoa wa Kigoma mara ya mwisho kutoa dawa za kichocho na minyoo ilikuwa mwa 2021.