Zaidi ya 100% ya watoto wapata chanjo ya polio Kigoma
25 October 2023, 09:11
Serikali kupitia idara ya afya Mkoa wa Kigoma imesema imefanikiwa kutoa chanjo ya polio kwa zaidi ya asiliamia 100 kwa watoto.
Na, Josephine Kiravu
Zaidi ya asilimia 100 ya watoto walio chini ya miaka minane wamepata chanjo ya polio katika zoezi liliofanyika September 21-24 huku idadi hiyo ikikadiriwa kuongezeka katika awamu ya pili ambayo inatarajia kufanyika mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba.
Nchini Tanzania, chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio hutolewa mara tu mtoto anapozaliwa anapofikisha umri wa wiki 6-14 na wakati wa kampeni maalum zinapohitajika na ni muhimu watoto wote kupata chanjo wakati wa kampeni ikiwemo waliokamilisha ratiba ya chanjo.
Mwezi Septemba mwaka huu ilifanyika kampeni ya chanjo ya polio kwa watoto walio chini ya miaka 8 ambapo zoezi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa huku matarajio yakiwa tofauti kwa awamu ya pili.
Hata hivyo changamoto hazikosekani kwani baadhi ya wazazi walikuwa na mitazamo hasi kuhusu chanjo hiyo ya polio ambayo ilitolewa kwa watoto walio na umri chini ya miaka 8.
Nao baadhi ya wazazi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji wamesema kukosekana kwa elimu miongoni mwao kuhusu ugonjwa wa polio ni chanzo cha baadhi yao kukataa watoto wao wasipate chanjo hiyo.
Tukumbuke chanzo ugonjwa wa polio husababisha ulemavu wa kudumu wa miguu,mikono au kifo,Na kila tone la chanjo ya polio humkinga mtoto dhidi ya ulemavu na kifo mpeleke mtoto apate chanjo.