Serikali, FAO wazindua kampeni ya upandaji miti Kigoma
16 October 2023, 18:03
Ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira nchini, serikali kwa kushirikiana na Shirika la Chakula Duniani FAO wamezindua zoezi la upandaji miti ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.
Na, Tryphone Odace
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO, kwa kushirikiana na serikali, limezindua kampeni ya upandaji miti ya matunda na rafiki wa maji wilayani Kasulu mkoani Kigoma, ili kusaidia uhifadhi wa mazingira na kuwa na uhakika wa matunda ya kula, kufuatia uharibifu mkubwa wa ukataji miti unaopelekea athari katika kuhifadhi mazingira.
Wakizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti elfu moja katika kijiji cha Kasangezi wilayani Kasulu iliyotolewa na shirika hilo, baadhi ya wananchi na viongozi wamesema kwa sasa mazingira yameathiriwa kutokana na vitendo vya ukataji wa miti.
Afisa kilimo wa FAO Tanzania Teresia Massoi amesema dunia inakumbwa na mabadiliko ya tabia nchi, hatua ambayo inatakiwa kuungwa mkono na mashirika na serikali ili kuhifadhi mazingira, huku mkurugenzi taasisi ya utafiti wa mbegu za kilimo Tanzania TARI Kihinga Kigoma Dk. Filson Kagimbo amesema juhudi hizo zitakuwa chachu ya kutunza mazingira.
Kwa upande wake, Mkurugenzi msaidizi Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dk. Nyamizi Bundala amesema kutokana na umuhimu wa maji ni lazima wadau na serikali kushirikiana ili kuhamasisha watanzania kuwajibika kupanda miti kwa wingi.