Wananchi Kakonko wakabiliwa na changamoto ya huduma za afya
13 October 2023, 13:25
Na Jame Jovin
Wananchi wa kijiji cha Nyakivyiru wilayani Kakonko mkoani Kigoma wameiomba halimashauri ya wilaya hiyo kuwajengea zahanati ili kuepuka kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 30 kufuata huduma za afya hali ambayo hupelekea vifo hasa kwa akina mama wajawazito, watoto na wazee.
Wakizungumza wakati wa mkutano wa hadhala wananchi wa kijiji cha Nyakivyiru ambacho hata hivyo bado hakijapata usajili kamili wamesema kuwa wamekuwa wakipata adha kubwa katika swala hilo la afya kutokana na umbali mrefu kutoka kijijini humo mpaka kufika kituo cha afya
Aidha kutokana na adha hiyo wananchi hao wameitaka serikali kutenga bajeti ya kujenga zahanati itakayosaidia katika huduma za awali kwa wananchi zaidi ya elfu nne wanaoishi katika kijiji hicho
Kwa upande wake diwani wa kata ya Gwarama bw. Fideli Nderego ameitaka serikali kukisajili kijiji hicho ili kurahisisha mipango ya kuleta huduma mbali mbali katika eneo hilo ikiwemo afya, elimu, maji na miundo mbinu mingine ya muhimu
Nae mkurugenzi mtendaji wa halimashauri ya wilaya ya Kakonko bw. Stephano Ndaki amesema kuwa swala la ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho litapewa kipaumbele mwaka wa fedha ujao ili kunusuru akina mama, watoto na wazee katika eneo hilo.