DC Uvinza apiga marufuku ramli chonganishi kwenye jamii
6 October 2023, 16:05
Serikali imesema itawachukulia hatua za kisheria wanaoendelea kupiga ramli chonganishi kwenye jamii wilayani Uvinza mkoani Kigoma.
Na Kadislaus Ezekiel
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dinna Mathamani amethibitisha kufariki watu watatu wakazi wa kijiji na kata ya Kazuramimba wilayani Uvinza mkoani Kigoma, baada ya vurugu zilizozuka kati ya wananchi na Jeshi la Polisi, kufuatia shinikizo la wananchi kutaka waganga wa jadi kuendelea kufanya ramli chonganishi.
DC Mathamani amesema wananchi wameendelea kuumizana kupitia ramli chonganishi zinazofanywa na waganga wa jadi maarufu KAMCHAPE, wakiamini kukamata wachawi walio katika maeneo yao.
Amesema wakati Jeshi la Polisi likizuia ramli chonganishi zilizokuwa zikifanyika kijiji na kata ya Kazuramimba, wananchi walipinga suala hilo kwa kutaka waganga wa jadi maarufu KAMCHAPE waendelee na kazi zao, ambapo hali hiyo ilipelekea vurugu na kusababisha vifo vya watu watatu.
Aidha DC Mathamani amesisitiza wananchi kujikita katika kufanya kazi na kupuuza masuala ya ushirikina, ambayo yanapelekea migogoro na machafuko kwa jamii, wakati watu wengi wakiendelea kuathirika.