Jamii mkoani Kigoma yatakiwa kujikinga na magonjwa ya mlipuko
25 August 2023, 17:24
Magonjwa ya mlipuko mkoani Kigoma yanaweza kudhibitiwa iwapo hatua mbalimbali zitachukuliwa na jamii.
Jamii mkoani Kigoma imetakiwa kushirikiana vyema na wadau wa sekta ya afya ili kuondoa tatizo la magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara. Mganga Mkuu mkoa wa Kigoma Dkt. Jesca Leba ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa kamati ya uelimishaji, uhamasishaji na ushirikishwaji wa jamii na kutoa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
Amesema bado kuna changamoto katika eneo la kujikinga na magonjwa ya mlipuko kwani hadi sasa baadhi ya watoto katika mkoa wa Kigoma wameugua ugonjwa wa kuhara na jitihada zinaendelea ili kuutokomeza ugonjwa huo unaotajwa kusababishwa na virusi.
Ameongeza kuwa idara ya afya pekee haitaweza kupambana na magonjwa ya mlipuko hivyo kila mwananchi anapaswa kuzingatia kanuni zote za afya huku akisisitiza kila kaya kuwa na choo bora.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Baraza na Wazee manispaa ya Kigoma Ujiji Mwl. Zuberi Kisongo amesema kuundwa kwa kamati hiyo itasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa watokanao na magonjwa ya mlipuko na itasaidia pia kufikisha kwa urahisi elimu kwa jamii ya namna ya kujilinda na magonjwa ya mlipuko.
Kamati hii ya Mkoa kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusu magonjwa ya mlipuko imejumuisha viongozi mbalimbali pamoja na wanahabari lengo likiwa ni kufikia jamii na kuipatia elimu ya namna ya kulijilinda na magonjwa ya mlipuko.