Aliyefariki miaka 29 iliyopita apatikana akiwa hai, akabidhiwa kwa ndugu Kibondo
13 July 2023, 13:15
Wananchi wilayani Kibondo mkoani Kigoma wametakiwa kutohusianisha tukio la kijana aliyefariki na kupatikana akiwa hai mkoani Tabora na imani za kishirikina.
Na James Jovin
Serikali wilayani Kibondo mkoani Kigoma imemkabidhi kijana Daniel Gastoni mwenye umri wa miaka 35 kwa ndugu zake waliopo kijiji cha Busunzu ikiwa ni siku chache baada ya kujitokeza na kusema kwamba alikufa kwa imani za kishirikina kwa zaidi ya miaka 29 iliyopita na kuonekana mkoani Tabora akiwa hai.
Kijana huyo amesema kuwa alikuwa amefariki katika mazingira ya kutatanisha na kupelekwa mkoani Tabora kwa njia za kishirikina ambapo alikuwa akifanyishwa kazi za kilimo na kuchunga mifugo kabla ya kuokolewa na Mungu na kisha kurejea wilayani Kibondo baada ya miaka 29 ya kufanyishwa kazi za nguvu pamoja na ushirikina.
Kijana huyo amekabidhiwa kwa familia yake na mkuu wa wilaya ya Kibondo Kanali Agrey Magwaza baada ya wasamalia wema kumpeleka ofisini kwake na kutoa maelezo ya awali juu ya changamoto iliyomtokea. Hata hivyo Kanali Magwaza amewataka ndugu, jamaa na majirani wa kijana huyo kutonyosheana kidole ama kuibua migogoro juu ya swala hilo.
Baba mzazi wa kijana huyo aliyepotea kwa zaidi ya miaka 29 amethibitisha kuwa mtoto huyo kweli ni wa kwake na alifariki miaka mingi iliyopita lakini ameshangaa kumuona tena akiwa hai.
Kwa upande wake kijana Daniel Gaston baada ya kukutanishwa na familia yake ameeleza kuwa amefurahi kuanza maisha mapya licha ya kutoonana na ndugu zake kwa zaidi ya miaka 29.
Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii kutoka halmashauri ya wilaya ya Kibondo Bi Neema Miti ameitaka jamii na ndugu wa kijana huyo kupokea yote yaliyotokea na kuyasahau lakini pia kuanza maisha mapya kwa kuwa karibu na kijana huyo aliyekumbwa na janga hilo .