Joy FM
Joy FM
9 February 2026, 08:18

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, amekemea vikali tabia ya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi sambamba na kujihusisha na uhalifu.
Na Kadislaus Ezekiel
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amekemea vikali tabia ya baadhi ya wakazi mkoani hapa kujichukulia Sheria mkononi sambamba na kujihusisha na uhalifu huku akisisitiza kuwa, serikali haitosita kuwakamata na kuchukua hatua kali dhidi ya wahusika wa vitendo hivyo.

Balozi Sirro ametoa kauli hiyo alipozungumza na wakazi katika Kitongoji cha Ilunde wilayani Uvinza mkoani hapa, kufuatia tukio la kifo cha mtu mmoja aliyefahamika kwa jila la Petro Kabasha (35), aliyeuwawa na watu ambao bado hawajafahamika wakati akilinda eneo la mwekezaji katika eneo tengefu la vitalu vya ufugaji wilayani humo.
Amesema eneo hilo limekuwa na historia ya migogoro ya muda mrefu ya ardhi ambayo pia imekuwa ikihusisha wakulima na wafugaji, ambapo amewataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi pale inapotokea mivutano kati yao bali waendelee kutumia mifumo ya kisheria kumaliza tofauti zao.

Amelitaka Jeshi la Polisi kuendesha zoezi maalum la kuwasaka watu wote wanaoendesha vitendo vya kihalifu na uvunjifu wa amani katika eneo hilo na kuwapeleka Mahakamani bila kuonea mtu au kuacha baadhi ya wahalifu wakiendelea kusumbua wananchi.
Upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Filemon Makungu, amesema uchunguzi unaendelea ili kuwabaini wahusika huku akisisitiza wananchi kushirikiana na Jeshi hilo kwa lengo la kuwafichua wahalifu wote waliohusika na tukio hilo.

Baadhi ya wakazi katika kitongoji hicho, wameliomba Jeshi la Polisi kuongeza nguvu na kuweka mikakati madhubuti katika kukabiliana na matukio hayo ili kudhibiti vitendo hivyo vya uvunjifu wa amani.