Joy FM
Joy FM
21 January 2026, 10:57

Katika jamii zetu kuna watu wenye mahitaji maalum kama vile wenye ulemavu wa viungo, kusikia, kuona au akili na watu hawa ni sehemu muhimu ya jamii na wana haki sawa na wengine hivyo basi ni wajibu wa jamii kuwasaidia ili waweze kuishi maisha yenye heshima na maendeleo.
Na Emmanuel Senny
Katika utekelezaji wa mpango wa uwajibikaji wa kijamii wa taasisi (Corporate Social Responsibility) na mchango wake katika kuboresha ustawi wa makundi yenye uhitaji maalumu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kigoma, imetoa misaada katika shule ya Msingi Kabanga Wilayani Kasulu ya watoto wenye mahitaji maalumu ikiwa na lengo la kurejesha shukrani kwa jamii.
TRA imetoa msaada huo January 20, 2026 baada ya kutembelea shule hiyo katika ziara iliyoongozwa na Meneja Msaidizi Huduma kwa Mlipakodi, Bw. Kwizera Ntibakazi, aliyemwakilisha Meneja wa Mkoa Bw. Beatus Nchota, pamoja na watumishi wengine wa TRA.

Katika ziara hiyo, TRA Kigoma imekabidhi misaada mbalimbali ikiwemo maharage, mchele, sukari, sabuni pamoja na mahitaji mengine ya msingi.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Meneja Msaidizi Huduma kwa Mlipakodi, Bw. Kwizera Ntibakazi amesema kuwa zoezi hilo ni ishara ya shukrani kwa walipakodi wa Mkoa wa Kigoma kwa ushirikiano wao mzuri na uzalendo katika kulipa kodi kwa hiari.
Bw. Kwizera amebainisha kuwa mapato yaliyokusanywa yameiwezesha TRA kuvuka malengo ya makusanyo kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya mwaka wa fedha 2025/2026.

“Walipakodi wetu wamekuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya Taifa. Kupitia msaada huu, tunarudisha sehemu ya shukrani zetu kwa jamii na kuonesha kuwa TRA ni mshirika wa maendeleo, si mkusanyaji wa mapato pekee. Hakika, pamoja tunajenga Taifa letu,” amesema Bw. Ntibakazi.
Kwa niaba ya watoto na uongozi wa shule hiyo, Bw. Kulwa Godluck ameishukuru TRA kwa mchango walioutoa na kuomba wasichoke kusaidia jamii, huku akieleza kuwa misaada hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kukidhi mahitaji ya msingi ya watoto hao na kuboresha mazingira yao ya malezi na kujifunzia.

Zoezi hilo linaonesha dhamira ya dhati ya TRA kuimarisha uhusiano chanya na jamii, kuchochea mshikamano wa kijamii, na kuendelea kujenga imani kwa walipakodi kupitia vitendo vinavyogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.