Joy FM
Joy FM
12 January 2026, 20:34

Serikali ya Mkoa wa Kigoma imesema wakimbizi kutoka Congo waliopo katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu wameendelea kuwa watulivu na kufuata sheria za ndani ya Nchi
Na Mwandishi wetu
Ujumbe wa Mawaziri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umewasili Mkoani Kigoma kwa lengo la kutembelea kambi ya kuhifadhi wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu ili kukutana na wakimbizi kutoka nchi hiyo.
Akizungumza mara baada ya kuupokea ujumbe huo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amesema wakimbizi kutoka nchi ya Congo, wamekuwa na utulivu na utii mkubwa wa sheria huku wakiwa na shauku kubwa ya kutaka kurejea katika nchi yao.

Upande wake Naibu Waziri wa Afrika Mashariki aliyeambatana na ujumbe huo, James Milya (Mb), amesema Tanzania imekuwa na mchango mkubwa katika kutafuta suluhu na amani ya nchi hiyo.
Naye Kiongozi wa Ujumbe huo ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Wizara ya Masuala ya Jamii, Hatua za Kibinadamu na Mshikamano, Eve Masudi amesema lengo la ziara yao ni kuwatembelea wenzao waliopo ukimbizini mkoani hapa ili kuwapa faraja na matumaini ya uwepo wa amani kwa nchi hiyo katika siku zijazo.

Ameendelea kusisitiza kuwa, dhamira kuu ya serikali ya Congo ni kushirikiana na mashirika ya umoja wa mataifa na kuhakikisha wanawarejesha wakimbizi hao nchini mwao ili kwenda kujenga taifa hilo lililoathiriwa na vita kwa muda mrefu.