Joy FM

Polisi Kigoma yathibitisha kumuua mtuhumiwa wa ujambazi Ziwa Tanganyika

16 December 2025, 11:10

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Filemon Makungu, Picha na Hamis Ntelekwa

Siku chache baada ya kuzinduliwa kwa oparesheni na doria katika ziwa Tanganyika kwa lengo la kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na majambazi kwa kuwapora zana za uvuvi wavuvi hatimaye wavuvi, mmoja apigwa risasi wakati wakitaka kutelekeleza jaribio la uhalifu ziwa Tanganyika

Na Emmanuel Matinde

Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma limethibitisha kumpiga risasi na kumuua mtuhumiwa wa ujambazi katika Ziwa Tanganyika, huku wengine kadhaa wakijitosa majini kufuatia majibizano ya risasi baina ya askari polisi na watu kadhaa wanaosadikiwa kuwa majambazi waliojihami kwa silaha dhidi ya polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Filemon Makungu, amesema hayo yamejiri katika tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha lililotokea jana Desemba 14, ambapo polisi wa doria wakiwa kazini walikabiliana na watu hao.

Sauti yaKamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Filemon Makungu

Aidha Kamanda Makungu,amesema katika tukio hilo wamekamata vitu mbali mbali ikiwemo silaha aina ya AK47, Injini za boti mbili, mtumbwi mmoja, nyavu tisa,simu za aina mbali mbali tisa, vyote vikiwa vimeporwa kwa wavuvi.

Bado haijafamika kama watuhumiwa hao akiwemo aliyepigwa risasi ni raia wa nchi gani lakini Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, SACP Filemon Makungu, amesema uchunguzi zaidi unaendelea, huku akisisitiza adhima ya kuutokomeza ujambazi katika Ziwa Tanganyika.

Sauti yaKamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Filemon Makungu

Hayo yamejiri ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, alipotangaza kuanza kwa doria za usiku na mchana zikihusissha vikosi vyote vya ulinzi na usalama ili kudhibiti uhalifu katika Ziwa Tanganyika.