Joy FM

Polisi, JWTZ waanza doria Ziwa Tanganyika

27 November 2025, 15:33

Askari wa Jeshi la Polisi na JWTZ wakiwa kwenye boti ndani ya Ziwa Tanganyika ikiwa ni sehemu ya doria kudhibiti uhalifu, Picha na Mwandishi wetu

Katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu ndani ya ziwa Tanganyika Jeshi la Pilisi kwa kushirikiana na JWTZ limezindua boti ya doria ndani Ziwa Tanganyika.

Na Mwandishi wetu

Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma kwa kushirikiana na jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) wameanza doria ya pamoja ya kudhibiti vitendo vya uhalifu na uporaji wa zana za uvuvi vinavyofanywa kwenye mwambao wa ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.

Mkuu wa wilaya Uvinza, Dinnah Mathamani amezindua zoezi hilo kwenye mwalo wa Muyobozi  kijiji cha Mwakizega wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ikiwa ni kutekeleza agizo la Mkuu wa mkoa Kigoma, Balozi Simon alilolitoa juzi katika kijiji cha Lubengera wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Mkuu wa wilaya Uvinza, Dinnah Mathamani amezindua zoezi hilo kwenye mwalo wa Muyobozi , Picha na Mwandishi wetu

Kuanza kwa doria hiyo ya pamoja kunakuja  baada ya malalamiko ya wavuvi na wachakataji wa mazao ya uvuvi kulalamika kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara ya wizi za zana za uvuvi unaofanywa na wahalifu wanaosadikiwa kutoka jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Akizundua zoezi hilo Mkuu huyo wa wilaya Uvinza amesema kuwa pamoja na kufanyika kwa doria hiyo pia vyombo vingine vya ulinzi na usalama ikiwemo idara ya uhamiaji vitaendelea na majukumu yake ikiwemo kukagua watu wote wanaoishi na kufanya kazi kwenye vijiji vya mwambao wa ziwa Tanganyika na watakaobainika kuishi bila kufuata taratibu watachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Uvinza, Fred Millanzi amesema kuwa Halmashauri hiyo inazo boti tano ambazo zitatolewa kusaidia  jukumu hilo zikigawanywa kulingana na maeneo ya kiutendaji yatakayoelekezwa.

Askari wa jeshi la Pilisi na JWTZ wakiwa kwenye boti ndani ya ziwa Tanganyika ikiwa ni sehemu ya doria kudhibiti uhalifu, Picha na Mwandishi wetu

Baadhi ya wananchi waliohudhuria uzinduzi huo akiwemo Zuberi Haruna mvuvi katika mwalo wa Muyobozi kijiji cha Mwakizega amesihukuru serikali hususani Mkuu wa mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro kwa hatua za kurudisha doria ya pamoja na polisi na jeshi la wananchi kwani hali ya ujambazi ziwa Tanganyika ilifikia kwenye hatua mbaya na wavuvi waliingia woga kununua vifaa vya thamani kuimarisha shughuli zao.