Joy FM
Joy FM
27 November 2025, 14:52

Watumishi wa umma Halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma wamepatiwa elimu ya kukabiliana na majanga ya moto
Na Hagai Ruyagila
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilayani Kasulu, mkoani Kigoma, limetoa mafunzo kwa watumishi wa umma wa Halmashauri ya Mji Kasulu kwa kuwajengea uwezo wa kukabiliana na majanga ya Moto yanapotokea.
Akizungumza wakati wa kutoa mafunzo hayo, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kasulu, Mrakibu Msaidizi Anthony Marwa, amesema mafunzo hayo yamelenga kuimarisha usalama mahali pa kazi kwa ajili na kuongeza uelewa wa namna ya kukabiliana na majanga ya moto yanayotokana na vyanzo mbalimbali.

Kuhusu Elimu kwa jamii na taasisi mbalimbali kupata elimu na uelewa wa matumizi sahihi ya vifaa vya kuzimia moto Marwa amesema wameendelea kutoa Elimu kwa watu mbalimbali ili kukabiliana na matukio ya dharura, ikiwemo majanga ya moto ambayo yanaweza kuleta madhara makubwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu, Mwl. Vumilia Simbeye, ameishukuru timu ya Zimamoto na kueleza kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka, kwani yatawajengea watumishi hao uelewa mpana kuhusu namna ya kujikinga, kuzuia na kukabiliana na majanga ya moto kazini na katika maeneo yao ya makazi.

Baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Mji Kasulu kutoka idara mbalimbali waliohudhuria mafunzo hayo wamesema yamekuwa na manufaa makubwa, ikiwemo kuongeza uelewa wao juu ya hatua sahihi za kuchukua wakati wa dharura na kutumia vifaa vya kuzima moto kwa usahihi.
