Joy FM

Wananchi watakiwa kufichua wahalifu ziwa Tanganyika

26 November 2025, 08:11

Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya Uvinza Mkoani Kigoma hasa wanaoishi maeneo ya mwambao wa ziwa Tanganyika wametakiwa kutoa taarifa na watu wanaojihusisha na ujambazi ndani ya ziwa Tanganyika

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Sirro ametembelea mwalo wa Lubengela katika Kijiji cha Msiezi Kata ya Sunuka Wilayani Uvinza mkoani hapa kwa lengo la kuzungumza na wakazi wanaoishi mwambao mwa Ziwa Tanganyika na kuwataka kuwafichua wahalifu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu katika ziwa hilo.

Mkuu wa Mkoa Kigoma akiwa ametembelea mwalo wa Lumbengela, Picha na Josephine Kiravu

Ziara hiyo imekuja kufuatia uwepo wa vitendo vya unyang’anyi wa vitendea kazi vya wavuvi zikiwemo injini, nyavu na vifaa vingine wakati wavuvi hao wakiwa katika shughuli zao za uvuvi.

Akizungumza na wakazi hao, Balozi Sirro amevielekeza vyombo vya Ulinzi na usalama mkoani hapa kuunganisha nguvu na kufanya doria usiku na mchana huku akiwataka wakazi wasio raia wa Tanzania ambao wanaishi kinyume cha Sheria kurejea katika nchi zao mara moja.

Wananchi wa maeneo ya Lubengela wakiwa katika mkutano wa Mkuu wa Mkoa Kigoma, Picha na Josephine Kiravu

Awali wakitoa malalamiko yao kuhusu uwepo wa matukio hayo, wakazi wa Kijiji hicho wameiomba Serikali kuongeza doria ndani na nje ya ziwa hususani katika maeneo ya vijiji vulivyopo pembezoni mwa ziwa  Tanganyika katika mkoa wa Kigoma.

Wamesema baadhi ya wanaoratibu matukio ya kiuhalifu wapo miongoni mwao jambo linalotoa mianya kwa raia wa kigeni kupata washirika katika kutekeleza uhalifu huo upande wa mkoa wa Kigoma.

Muonekano wa mwalo wa Lubengela mwambao wa ziwa Tanganyika, Picha na Josephine Kiravu