Joy FM
Joy FM
19 November 2025, 12:22

Na Lucas Hoha
Kikundi cha umoja wa majirani wanaume waishio Kata ya Kibirizi Mtaa wa Buronge Manispaa ya Kigoma Ujiji wametoa msaada wa vitu mbalimbali katika kituo cha kulelea wazee wasiojiweza cha Silabu lengo likiwa ni kuonesha umoja katika kuisaidia jamii ya watu wenye mahitaji.
Wakikabidhi msaada huo baadhi ya viongozi wa kikundi hicho akiwemo Zabron Yusufu na Octavian Lutasha wamesema wamedhamiria kufanya shughuli za kijamii na kuyafikia makundi mbalimbali yenye uhitaji wakiwemo yatima, wazee na wagonjwa.
Awali akipokea msaada huo, Afisa ustawi wa jamii katika makazi ya wazee wasiojiweza Fred David pamoja na mambo mengine amesema wazee hao wanamahitaji ya vitu mbalimbali ambapo ametoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia
Baadhi ya wazee wanaolelewa katika kituo hicho, wameshukuru kikundi cha umoja wa majirani wanaume wa Buronge kuwapatia msaada huo, huku wakitaja baadhi ya mahitaj yao ambayo wangependa jamii iwasaidie ikiwemo mavazi na chakula.