Joy FM

Katibu tawala Kigoma aongoza wananchi kupiga kura

29 October 2025, 11:30

Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa, Picha na Josephine Kiravu

Wananchi na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma wamejitokeza kupiga kura leo katika maeneo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa matakwa ya kikatiba ya kuchagua viongozi wao

Na Josephine Kiravu

Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa hii leo Oktoba 29,2025 amewaongoza wananchi wa mkoa wa Kigoma kupiga kura na kutimiza wajibu wao na kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka miatano.

Akiwa katika kituo cha kupiga kura eneo la Kigoma mjini ilipo ofisi ya mtendaji wa kata ya kigoma mjini Katibu Tawala Hassan Rugwa amewahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura huku akiwathibitishia wananchi wote kwamba Tume huru ya uchaguzi imeweka mazingira rafiki na utaratibu mzuri na kwamba vituo ni vingi ambavyo vinawezesha mpiga kura kutotumia muda mwingi kusimama kituoni.

Sauti ya Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Hassan Rugwa

Kwa upande wake, Kamanda wa polisi mkoani Kigoma SACP Filemon Makungu amewahakikishia wananchi amani na utulivu kipindi chote cha zoezi la kupiga kura na kwamba ulinzi umeimarishwa kwenye vituo vya kupigia kura.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma SACP Filemon Makungu

Naye mgombea wa kiti cha Udiwani kata ya Kigoma mjini Hussein Kalyango amesema mpaka sasa zoezi la uchaguzi linaendelea vyema licha ya uwepo wa dosari chache ambazo anaamini zitapatiwa ufumbuzi.

Viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania DR Philip Mpango akiwa katika kijiji cha Kasumo wilayani Buhigwe ameshiriki kupiga kura ya kuchagua Rais ,wabunge na madiwani.

Zaidi ya watu milioni 37.6 wanatarajiwa kupiga kura hii leo ambapo kati yao milio 36.65 wapo Tanzania Bara na 996,000 wapo Zanzibar, itakumbukwa huu ni uchaguzi wa saba tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.