Joy FM

Wenye ulemavu Kasulu kuchangamkia mikopo

24 October 2025, 15:32

Watu wenye ulemavu wakiwa katika hafla ya ugawaji wa viti mwendo, Picha na Hagai Ruyagila

Halmashauri ya mji Kasulu Mkoani Kigoma imewataka watu wenye ulemavu kujitokeza na kuchangamkia mikopo inayotolewa kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Na Hagai Ruyagila

Watu wenye Ulemavu katika halmashauri ya Mji Kasulu Mkoani Kigoma wameshauriwa kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri hiyo ili kujikwamua na kujiletea maendeleo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu Mwl, Vumilia Simbeye wakati akizungumza na vyombo vya habari Mjini Kasulu mkoani Kigoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kasulu Mwl, Vumilia Simbeye, Picha na Hagai Ruyagila

Mwl. Simbeye amesema serikali imeendelea kutoa mikopo kupitia halmashauri mbalimbali nchini, kama njia ya kuwawezesha wananchi wote bila ubaguzi kupata fursa za kiuchumi na kupiga hatua katika maendeleo yao.

Aidha Mwl. Simbeye amesema kuwa kwa upande wa watu wenye mahitaji maalum, si lazima kuunda kikundi cha watu watano au zaidi ili kupata mkopo bali hata mtu mmoja anaweza kupewa mikopo hiyo, mradi tu awe mwaminifu katika urejeshaji wa fedha hizo kwa wakati.

Watu wenye ulemavu wakiwa katika hafla ya ugawaji wa viti mwendo, Picha na Hagai Ruyagila

Pia amewataka watu wenye ulemavu kutumia fursa hiyo vizuri kwa kuanzisha miradi yenye tija itakayowawezesha kujitegemea na kuondokana na utegemezi.

Baadhi ya Watu wenye mahitaji maalum kutoka halmashauri ya Mji Kasulu wamepongeza namna serikali inavyo wajali wakisema kuwa ni hatua muhimu inayowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na kukuza kipato chao.

Mikopo hiyo itawasaidia kuboresha maisha yao na kuchochea maendeleo ya jamii kwa ujumla.