Joy FM
Joy FM
22 October 2025, 09:51

Watu wenye mahitaji maalum hawana budi kushirikishwa kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi ikiwa ni sehemu ya kujenga jamii jumuishi
Na Hagai Ruyagila
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umetoa msaada wa viti mwendo 11 vyenye thamani ya shilingi milioni 4.5 kwa Shirika la Sauti Yetu Foundation kwa ajili ya kuwagawia watu wenye mahitaji maalum katika Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma.
Hafla ya ugawaji wa viti mwendo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari Bongwe iliyopo Mjini Kasulu na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wawakilishi wa taasisi pamoja na wanufaika wa msaada huo.
Akizungumza katika hafla hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Sauti Yetu Foundation kutoka jijini Dodoma BW. Raphael Mabula amesema msaada huo unalenga kuwawezesha watu wenye mahitaji maalum kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga jamii jumuishi isiyomwacha mtu nyuma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mji Kasulu Mwl, Vumilia Simbeye ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika tukio hilo amelipongeza shirika hilo kwa moyo wao wa huruma na upendo kwa jamii hususan kwa watu wenye mahitaji maalum.
Amewasihi pia wazazi na walezi kutowaficha watoto wao wenye ulemavu majumbani, bali wawape fursa ya kushiriki katika shughuli za kijamii na kupata haki sawa na watoto wengine.

Baadhi ya wazazi na walezi wa watoto waliopokea msaada huo akiwemo Amina Bakari wametoa shukrani zao za dhati kwa shirika hilo kuwa msaada huo umewapa matumaini mapya na kuongeza uwezo wa watoto wao kushiriki katika maisha ya kila siku.

Shirika la Sauti Yetu Foundation linaendelea na juhudi zake za kuwasaidia watu wenye uhitaji katika maeneo mbalimbali nchini likilenga kuboresha maisha na kutoa fursa sawa kwa makundi yote ya jamii.