Joy FM

Wananchi watakiwa kutambua vituo vya kupigia kura Kasulu

22 October 2025, 09:36

Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kasulu mjini Nurfus Aziz, Picha na Hagai Ruyagila

Wakati ikiwa imebaki wiki moja kabla ya kufika siku ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika oktoba 29, 2025 wananchi wameaswa kufuatilia taarifa na vituo vyao mapema ili waweze kuhudhuria kupiga kura

Na Hagai Ruyagila

Wananchi katika Halamashauri ya mji wa Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kutambua mapema vituo vyao vya kupiga kura kabla ya siku ya uchaguzi ili kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza siku ya kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu.

Akizungumza na vyombo vya Habari msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kasulu mjini Nurfus Aziz ameeleza kuwa taratibu za uchaguzi mkuu zimekamilika hivyo wananchi wanalojukumu la kuhakikisha wanashiriki katika uchaguzi huo oktoba 29 mwaka huu ili kutimiza haki yao ya kikatiba.

Amesema kila kituo cha kupiga kura wameweka taarifa mbalimbali ikiwemo mfano wa karatasi za kupiga kura yenye majina na picha za kila mgombea mgombea pamoja na nembo zao za vyama vya siasa kwa uchaguzi wa rais wabunge na madiwani ili kuwajengea uelewa wananchi namna ya kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu.

Kwa upande wake Afisa uchaguzi Jimbo la kasulu mjini Bw. Daniel Kaloza amesema wataendelea kutimiza wajibu wao kama maelekezo ya tume huru ya uchaguzi yanavyoelekeza pia ameendelea kutoa msisitizo wake kwa wananchi kuhakikisha wanafika vituo vya kupiga kura walivyojiandikisha kwa ajili ya kuchagua viongozi wao

Viongozi wa vyama vya siasa wilayani Kasulu akiwemo mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM Mbelwa Chidebwe, Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo Haruna Kwasakwasa na Katibu wa chama cha Wananchi CUF Ahmad Dugala licha ya kupongeza maandalizi yaliyofanywa na tume huru ya uchaguzi wamesema wataendelea kuhamasisha wananchi kwenda kupiga kura ili kutekeleza haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanao wahitaji.

Viongozi wa vyama vya siasa Wilayani Kasulu, Picha na Hagai Ruyagila