Joy FM
Joy FM
16 October 2025, 23:33

Licha ya Serikali na shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kuhamasisha wakimbizi waliopo katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu tangu mwaka 2017 na kuonekana zoezi la kurejea nchini kwao kwa hiari kusuasua sasa mwarobaini wa kuwarudisha wakimbizi hao ni pamoja na kuwafutia hadhi ya kuwa mkimbizi ili waweze kurejea nchini kwao kwani tayari Burundi ipo salama
Na Mwandishi wetu
Serikali ya Tanzania na shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR zimetangaza kufuta hadhi ya ukimbizi kwa wakimbizi kutoka Nchini Burundi wanaoishi katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu iliyopo Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma kwani tayari muda wa kuishi nchini kama wakimbizi umeisha na hivyo hawana budi kuridi nchini kwao kutokana na usalama na amani uliopo nchini Burundi.
Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa huduma idara ya wakimbizi, Wizara ya mambo ya ndani ya nchi, Sudi Mwakibasi wakati akizungumza na wakimbizi hao ambapo mesema tayari uhamasisho wa wakimbizi kurudi kwao umeshafanyika na hivyo hawana budi kurudi na kwenda kuijenga nchi yao kwani imetulia na amani ya kutosha ili waweze kujiletea maendeleo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amewataka wakimbizi hao waweze kurudi kwao ili wakaendelee na shughuli za kiuchumi katika taifa lao kwani kuendelea kuishi kambini kunawafanya watoto na vijana kukosa huduma muhimu na kupoteza malengo yao ya nchi yao.
Mwakilishi mkazi wa shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Babra Dotse amesema kuwa kulingana na utafiti walioufanya wamebaini kuwa wakimbizi hawana budi kurudi kwao kwani tayari kuna amani ya kutisha licha ya kuwa wengi wao wanaonyesha kuhitaji kwenda nchi ya tatu.

Naye balozi wa Burundi katika ubalozi mdogo wa Kigoma Kekenwa Jeremiah amewaasa wakimbizi kutoka Burundi waweze kurejea nyumbani kwao kwani machafuko yaliyosababisha wakimbie nchi yao yameshaisha baada ya makubaliano ya mkataba wa kumaliza tofauti kati ya makundi yaliyokuwa yakihasiamiana na sasa umoja na mshikamano upo vizuri nchini humo.

Aidha Balozi Kekenwa amesema kuwa kwa sasa Burundi kuna amani ya kutosha na maendeleo yanaendelea kukua na kuongeza uchumi wa jamii yao na Taifa kwa ujumla.