Joy FM
Joy FM
16 October 2025, 19:55

Na Hagai Ruyagila
Chama cha NCCR – Mageuzi kimewataka wananchi wote wenye nia ya kuanzisha maandamano kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, kuachana mara moja na mpango huo, kikisisitiza kuwa maandamano hayo yanaweza kuhatarisha amani na usalama wa taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Idara ya Sheria Katiba na Haki za Binadamu Taifa wa chama hicho, Faustin Sungura, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Kasulu, mkoani Kigoma.
Faustin amesema ni muhimu kwa vyombo vya dola kuchukua hatua stahiki dhidi ya wale wote wanaopanga maandamano yasiyo halali, kwani hatua hizo hazina tija kwa maendeleo ya nchi.

Ameongeza kuwa njia bora ya kushiriki mchakato wa kidemokrasia ni kwa wananchi kujiandaa kwa utulivu kushiriki kikamilifu katika upigaji kura ili kuwachagua viongozi wanaowataka kwa njia ya amani.
Katika hatua nyingine, Sungura amepongeza kauli ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, kusaidia watu wenye ulemavu, akisema ni jambo linalogusa mioyo ya wengi hivyo, ameomba vyama vyote kuwaondoa wagombea wao wa ubunge katika Jimbo la Kasulu Vijijini, ili kumpisha mgombea wao, Yohana Benjamini mtu mwenye ulemavu agombee bila kupingwa kama ishara ya kuunga mkono ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kasulu wameunga mkono kauli ya NCCR Mageuzi, wakieleza kuwa maandamano hayawezi kuleta mafanikio yoyote, bali yanaweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo.