Joy FM
Joy FM
25 September 2025, 08:26

Jamii Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma imehimizwa kujiunga na Bima ya Afya ili kujihakikishia huduma bora za matibabu kwa wakati wa changamoto za kiafya.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa wilaya ya Kasulu Bw, Selemani Malumbo wakati akizungumza na wazazi na walezi wa kata ya Nyansha.
Bw Malumbo, amesema kuwa na bima ya afya ni hatua muhimu ya kuhakikisha familia inapata matibabu bila usumbufu wa kifedha.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa meneja wa mfuko wa Taifa ya Bima ya afya (NHIF) mkoa wa Kigoma Bw. Deogratius Chakupewa amesema mfuko huo uko tayari kutoa huduma za matibabu kwa gharama nafuu hususan kwa wanafunzi wa shule zilizosajiliwa nchini kote.
Baadhi ya Wazazi na walezi wamepongeza jitihada za serikali na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo ili kuhakikisha watoto wao, pamoja na wao wenyewe wanapata huduma za afya kwa wakati.
Mpango huu wa kujiunga na Bima ya Afya unalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza gharama kubwa zinazotokana na matibabu hasa kwa familia zenye kipato cha chini.