Joy FM
Joy FM
11 September 2025, 13:39

Wito umetolewa kwa wagombea kuhakikisha wanafanya kampeni za ustaarabu na kuheshimu kanuni na sheria za Nchi ili kuepuka kusababisha vurugu kwa Taifa
Na Hagai Ruyagila
Wagombea wa nafasi mbali mbali za uongozi katika wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wameshauriwa kuhakikisha kampeni zao zinafanyika kwa amani, bustarabu na ustarabu ili kuendeleza utulivu uliopo Nchi.
Wito huo umetolewa na Askofu wa kanisa la FPCT Jimbo la Kasulu, Shedrack Bunono wakati akizungumza na viongozi wa serikali, viongozi wa dini na wa vyama vya siasa Mjini Kasulu.
Askofu Bunono amewasisitiza wanasiasa kutumia lugha ya staha na kuepuka maneno ya uchochezi ambayo yanaweza kusababisha migogoro au kuleta sintofahamu miongoni mwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha Wananchi CUF wilaya ya Kasulu Ndg. Vedasto Kagina ameeleza kuwa wamejipanga kuhakikisha wanafanya kampeni kwa ustarabu, kwa kufuata sheria na miongozo ya tume huru.
Nao baadhi ya Wananchi wa wilaya ya Kasulu wameunga mkono kauli hizo na kuwataka wagombea wote kuzingatia sheria na taratibu za uchaguzi ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Wito huu unakuja katika kipindi ambacho nchi inajiandaa kuelekea uchaguzi mkuu, ambapo wadau mbalimbali wanaendelea kuhimiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na umoja wa taifa.
