Joy FM

RC Kigoma ahimiza viongozi wa dini kuhubiri amani

10 September 2025, 09:28

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP Mstaafu Balozi Simon Sirro, Picha na Hagai Ruyagila

Serikali ya Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na Serikali Kuu imesema itaendelea kusimamia Sera na mikakati ya kudumisha amani, usalama na Maendeleo kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma.

Na Hagai Ruyagila

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP Mstaafu Balozi Simon Sirro, ametoa wito kwa viongozi wa dini mkoani humo kuendelea kuhubiri amani,  mshikamano na Maadili mema ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa taifa lenye utulivu na usalama wa kudumu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Akizungumza katika kongamano la amani lililofanyika Mjini Kasulu kwa lengo la kuombea uchaguzi mkuu mwaka huu, Balozi Sirro amesema kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye maadili mema na katika kuchochea mshikamano wa kitaifa.

Baadhi ya viongozi wa dini walikuwa kwenye kongamano la kuombea Taifa, Picha na Hagai Ruyagila

Kupitia Kongamano hilo amesisitiza viongozi wa dini kuhamasisha maadili mema kwa wananchi ili kuendelea kuimarisha hali ya amani nchini.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, IGP Mstaafu Balozi Simon Sirro

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu amezungumzia suala la ulinzi na usalama katika wilaya hiyo sambamba na kuwashukuru viongozi wa dini kwa namna wanavyoshirikiana na serikali katika matukio mbalimbali wilaya humo.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu
Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu, Picha na Hagai Ruyagila

Askofu wa kanisa la FPCT Jimbo la Kasulu Shedrack Bunono amesema kuwa taasisi za dini zitaendelea kutoa elimu ya maadili na upendo kwa waumini wao ili kuimarisha utulivu katika jamii.

Sauti ya Askofu wa kanisa la FPCT Jimbo la Kasulu Shedrack Bunono
Askofu wa kanisa la FPCT Jimbo la Kasulu Shedrack Bunono, Picha na Hagai Ruyagila

Naye Katibu wa maridhiano wilaya ya Kasulu Shekhe Nassibu Rajabu ametoa wito kwa jamii kuwa na upendo na kuvumilia ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa taifa.

Sauti ya Katibu wa maridhiano wilaya ya Kasulu Shekhe Nassibu Rajabu

Kongamano hilo limekusanya viongozi mbalimbali wa dini, watendaji wa serikali na wanajamii kwa lengo la kuimarisha maombi ya pamoja kuhusu umuhimu wa amani kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.