Joy FM
Joy FM
8 September 2025, 09:38

Mgombea ubunge wa jimbo la Kigoma mjini kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amewataka wapiga kura katika jimbo hilo kumpa kura nyingi za ndiyo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu ili aweze kurudi bungeni kuwatumikia lakini pia kulinda heshima ya bunge hilo.
Na Tryphone Odace
Chama cha ACT Wazalendo Jimbo la Kigoma Mjini kimezindua rasmi kampeni zake za kuwania kutwaa jimbo hilo na kufanya mkutano wake wa kwanza wa kumnadi mgombea wake Zitto Zuberi Kabwe.
Akizungumza na mamia ya wafuasi wa chama hicho pamoja na wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa kampeni hizo katika viwanja vya Mwami Ruyagwa vilivyopo kata ya Gungu Manispaa ya Kigoma Ujiji, mgombea ubunge wa ACT Wazalendo Jimbo la Kigoma Mjini Zitto Kabwe, amewaomba wamtume tena bungeni akafanye kazi ya kuwawakilisha na kujenga heshima ya watu wa Kigoma.

Zitto amewataka wakazi wa jimbo la Kigoma Mjini kutofanya makosa ya kuchagua mgombea wa chama kingine, akisisitiza kuwa huu ni wakati ambao jimbo hilo linahitaji kiongozi kama yeye ili kuendeleza miradi iliyoanzishwa na chama chake kilipoongoza halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji kati ya mwaka 2015 na 2020.
Aidha Zitto Kabwe amewataka wapiga kura katika jimbo la Kigoma Mjini kutumia miezi hii miwili ya kampeni kutafakari kwa kina aina ya kiongozi wanayemtaka ili kufanya uamuzi sahihi ifkapo Oktoba 29,2025.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo Abdul Nondo, amewataka vijana na wananchi wote wa jimbo la Kigoma Mjini, kumchagua Zitto Kabwe ili awawakilishe bungeni kwa sababu tayari ameonyesha kuwa ndiye anayeweza kufanya hivyo.
