Joy FM
Joy FM
20 August 2025, 16:08

Wagombea waendelea kuchukua fomu za kugombea na kuahidi kushirikiana na wananchi
Na HagaiRuyagila
Wananchi wa Kata ya Mwilamvya, wilayani Kasulu Mkoani Kigoma wametakiwa kudumisha umoja, mshikamano na kuachana na makundi ya kisiasa yanayoweza kusababisha migogoro, Badala yake wametakiwa kushirikiana katika juhudi za kuleta maendeleo kwenye kata hiyo.
Wito huo umetolewa na mgombea mteule wa nafasi ya Udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mwilamvya, Jimbo la Kasulu Mjini, Bw. Emmanuel Gamuye, mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika Ofisi za INEC, kata ya Mwilamvya.
Bw. Gamuye amesema kuwa baada ya kukamilika kwa mchakato wa ndani wa chama uliohusisha upatikanaji wa wagombea wa nafasi za uongozi, ni wakati sasa kwa wananchi na jamii kusahau tofauti zao za kisiasa na kuungana kwa lengo la kujadili na kutekeleza mipango ya maendeleo ya kata hiyo.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Kata na pia Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Kasulu, Mwl. Casiani Costa Mbajije, amewashukuru wana chama wa chama hicho kumuunga mkono mgombea huyo aliyechukua fomu na kuwasihi kuendelea kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha hakuna migawanyiko yotote ya kisiasa itakayoibuka ndani ya chama.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwilamvya wamewataka wenzao kuwa na utulivu na kujiepusha na ushabiki wa kisiasa usio wa lazima, huku wakisisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi wanaojali maendeleo ya wananchi wote maana kiu yao ni kuendelea kupata maendeleo zaidi katika kata hiyo.
Uchaguzi Mkuu unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, ambapo wananchi watapata fursa ya kuchagua viongozi wanaowaamini kuwatumikia katika nafasi mbalimbali za uongozi