Joy FM
Joy FM
12 August 2025, 11:20

Kuelekea uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais, wakristo wameaswa kuendelea kuombea uchaguzi huo ili uweze kufayika kwa amani na utulivu
Na Hagai Ruyagila
Waumini wa Dini ya Kikristo katika Wilaya ya Kasulu, Mkoani Kigoma, wametakiwa kuendelea kuliombea taifa la Tanzania kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba Mwaka huu, ili uchaguzi huo ufanyike kwa amani, utulivu na hatimaye kuwapata viongozi sahihi watakaosaidia kuimarisha mshikamano wa kitaifa na maendeleo ya taifa.
Wito huo umetolewa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la FPCT Hwazi, lililopo katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Mch. Eliya Mafyondi, wakati wa ibada maalum ya maombi iliyofanyika kanisani hapo kwa ajili ya kuliombea taifa kipindi hiki muhimu cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Katika hotuba yake, Mchungaji Mafyondi amewasihi waumini na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuliombea taifa si tu kabla ya uchaguzi, bali pia baada ya uchaguzi huo ili kudumisha amani, mshikamano wa kitaifa, na maendeleo endelevu.
Amesisitiza kuwa maombi ni silaha muhimu ya kiroho inayoweza kusaidia kulinda umoja wa kitaifa, hata katika mazingira ya tofauti za kisiasa, kijamii au kiitikadi.
Kwa upande wao, baadhi ya waumini wa Kanisa la FPCT Hwazi wamesema wako tayari kuiombea Tanzania na kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani. Wameeleza kuwa uchaguzi wa utulivu ndio msingi wa mafanikio ya taifa, huku wakibainisha umuhimu wa kuwa na viongozi wenye maono, uadilifu na moyo wa kizalendo.
Maombi hayo yamebeba ujumbe mzito wa mshikamano wa kitaifa, uzalendo na hitaji la kuwa na viongozi wanaotanguliza maslahi ya taifa. Pia wamesema ni jukumu la kila raia kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, na haki na wenye kuleta matumaini mapya kwa Watanzania.