Joy FM
Joy FM
6 August 2025, 12:33

Wito umetolewa kwa wadau mbaimbali na mashirika kuendelea kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili waweze kufikia ndoto zao.
Na Hagai Ruyagila
Katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita katika kuboresha sekta ya afya nchini, Taasisi ya Usilie Tena yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam, imetoa msaada wa kadi za bima ya afya kwa baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Rungwe Mpya na Kalema, zilizopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Bi. Egra Kamugisha, amesema hatua hiyo inalenga kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu ambao wanakumbwa na changamoto ya kukosa huduma bora za afya kutokana na hali ngumu ya maisha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu ameishukuru Taasisi hiyo kwa moyo wa huruma waliouonesha kwa watoto hao, na kumuombea heri mkurugenzi wa taasisi hiyo kwa kazi njema anayofanya kwa jamii.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kalema, Mwalimu Hellena Kabonye, pamoja na Mwalimu wa Kitengo cha Elimu Maalum kutoka Shule ya msingi Rungwe Mpya, Mwalimu Agatha Chendro, wamesema msaada huo wa bima ya afya utasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi hao kwa kuwa hawatalazimika kukosa masomo kutokana na maradhi.
Baadhi ya wazazi na watoto waliopokea bima hizo wameonesha furaha na kutoa shukrani kwa mdau huyo wa elimu, huku wakihimiza malezi bora na kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila vikwazo.

Hatua hii ya Taasisi ya Usilie Tena ni mfano hai wa ushirikiano kati ya serikali na wadau binafsi katika kuhakikisha kila mtoto anapata haki ya msingi ya afya na elimu, hasa wale wenye uhitaji maalum.