Joy FM
Joy FM
18 June 2025, 15:36

Kuelekea uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi oktoba mwaka huu, Wakristo wametakiwa kuendelea kuombea amani na utulivu
Na Hagai Ruyagila
Waumini wa dini ya Kikristo wametakiwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi pamoja na kuuombea uchaguzi huo ufanyike kwa amani na utulivu.
Wito huo umetolewa na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Western Tanganyika, Mhashamu Emmanuel Bwatta, wakati wa ibada maalum ya Sakramenti ya Kipaimara na uwekaji wa jiwe la msingi kwenye jengo jipya la Kanisa la Anglikana Murusi, linaloendelea kujengwa kwa ajili ya ibada.

Askofu Bwatta amesema ni jukumu la kila muumini kuombea uchaguzi huo ili ufanyike kwa amani, lakini pia kwa wale wanaohisi kuitwa na Mungu kuongoza, wachukue hatua ya kuchukua fomu na kugombea nafasi za uongozi kwa ajili ya kuliletea taifa maendeleo na kudumisha maadili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanisa la Anglikana Kanda ya Kasulu Mjini, Mchungaji Canon Laurent Magogwa, ameeleza umuhimu wa uchaguzi huo na kuwasihi kuchagua viongozi bora.
Baadhi ya waumini wamesema wana matumaini kuwa uchaguzi huo utafanyika kwa amani, huku wakitoa maoni tofauti kuhusu ushiriki wao katika siasa na mchakato wa uchaguzi.
Ibada hiyo ya kipekee imehudhuriwa na waumini kutoka maeneo mbalimbali ya Kasulu na wageni wengine kutoka nchini Marekani na Uingereza ikiwa ni ishara ya mshikamano na umoja wa kiroho.