Ukweli wote zoezi la uandikishaji wapiga kura Kigoma
23 October 2024, 12:18
Viongozi wa siasa mkoani Kigoma kupitia umoja wa vyama vya siasa mkoani hapa wameeleza kuridhishwa na zoezi la uandikishaji kwenye daftari la wakazi kwa ajili ya kupata sifa ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27,2024.
Na, Josephine Kilavu
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa kamati maalum ambayo iliundwa kwa lengo la kutembelea halmashauri za mkoa ikiwemo Kigoma Manispaa,Kigoma DC, Kasulu TC, Kasulu DC,pamoja na Buhigwe ili kujionea hali ilivyo kufuatia kuzuka kwa taarifa zinazoeleza mwitikio hasi wa wananchi kwenye zoezi hilo.
Kwa upande wake katibu wa kamati hiyo Rajbu Nyambaro ambaye pia ni katibu wa chama cha NCCR Mageuzi amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kwenye zoezi hilo huku akiwataka makatibu wa vyama vya siasa kuendelea kuhubiri siasa ambazo hazitaleta uvunjifu wa amani.
Kwa upande wao wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Musa Habibu katibu wa Ada Tadea na Amani Salum katibu wa AFP wamesema wameridhishwa na mchakato mzima kwenye zoezi la uandikishaji na kuwataka wakazi waliojiandikisha kutumia haki yao ya kikatiba muda utakapowadia kumchagua kiongozi bora atakaewasilisha vyema changamoto zao.
Zoezi la uandikishaji wakazi kwenye daftari la mkazi lilianza Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu ambapo wakazi ambao wamefikisha umri wa zaidi ya miaka 18 wamepata fursa ya kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27 mwaka huu