Joy FM

watuhumiwa wizi wa maji mikononi mwa polisi Kigoma

22 August 2024, 15:05

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Kigoma/Ujiji (KUWASA), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, wameendesha operesheni na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wa wizi wa maji waliokuwa wakiiba kwa zaidi ya miaka kumi.

Katika operesheni hiyo, Gidion Kiriba, mkazi wa Mtaa wa Mlole, amekamatwa baada ya kugundulika kuwa ameunganisha bomba ndani ya nyumba yake kinyume na utaratibu, licha ya kukatiwa maji kwa muda mrefu.

Gidion Kiriba

Mtuhumiwa wa pili, Edina Samwel, amekamatwa baada ya kugundulika kuwa ameunganisha bomba katika kibanda chake, ambacho hutumia kwa kufunga na kufungua kufuli kulingana na mahitaji yake ya huduma ya maji.

Edina Samwel

Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa KUWASA, Philippo Funga, amethibitisha kuwa watuhumiwa wote watafikishwa kwenye vyombo vya dola kwa ajili ya hatua za kisheria na operesheni za kubaini na kukamata wahalifu wa wizi wa maji zinaendelea.

Philippo Funga

Kwa mujibu Sheria namba 5 ya huduma za maji na usafi wa mazingira ya mwaka 2019 mtu atakayekutwa anaharibu au kuingilia miundombonu ya maji adhabu yake ni faini isiyopungua Shilingi laki tano na isiyozidi Milioni 50 au kifungo kisichopungua miaka miwili na kisichozidi miaka mitano au vyote kwa pamoja.