Neema yawashukia wakulima wa mpunga kasulu
6 May 2024, 15:58
Serikali imeeleza kuwa wakulima wataendelea kuneemeka na mavuno yenye tija iwapo watazingatia maelekezo ya wataalamu wa kilimo juu ya kilimo chenye tija na ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.
Na Timotheo Leonard – Kasulu
Wakulima wa zao la Mpunga katika Kata ya Titye Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma wameshauriwa kulima kilimo chenye tija kwa kuzingatia matumizi ya mbolea.
Ni wakulima wa Kata ya Titye wakicheza kwa furaha katika siku ya Wakulima wa zao la Mpunga katika eneo hilo kupitia mradi wa kuchochea mapinduzi ya kilimo kwa njia ya urutubishaji wa mazao ya nafaka Afrika kwa ushirikiano wa Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania TARI
Mradi huu wa kuchochea mapinduzi ya Kilimo kwa njia ya urutubishaji wa mazao ya nafaka Afrika unaofadhiliwa na taasisi ya APNI ya nchini Kenya kwa kushirikiana na TARI ukilenga kuhakikisha wakulima wanatumia kanuni bora za kilimo
Bw:Nicholaus Fedrick Kibabi na Daudi Martin Mubingo ni wakulima wa mpunga ambao wanaeleza manufa ya kilimo hicho cha kisasa
Penye mafanikio hapokosi kuwa na changamoto kama wanvyoeleza baadhi ya wakulima, huku kiu yao ikiwa ni upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakati.
Diwani wa Kata ya Titye Eliazar Mizigiro amesema Skimu ya umwagiliaji wa kilimo cha Mpunga katika kata hiyo ina zaidi ya wakulima 700 ambao matamanio yao ni kuona TARI inawapatia mbegu iliyo bora na kusimamia swala la elimu ya kilimo cha kisasa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa Kilimo Tanzania TARI -KIHINGA Dkt. Filson Kagimbo amesema wakulima hawana budi kufanya ulinganifu wa kilimo cha kisasa cha mpunga na kilimo cha kawaida ili waweze kulima kwa tija kwa manufaa yao.
Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kasulu katika sherehe hizo za wakulima wa mpunga, Katibu tawala wa Wilaya ya Kasulu Bi. Theresia Mtewele amesema Serikali itahakikisha mbolea inafika kwa wakati na changamoto nyinginezo wataangalia namna ya kuzitatua kwa wakati.