Wananchi watakiwa kuulinda na kudumisha muungano
26 April 2024, 16:19
Wananchi wametakiwa kuendelea kuuenzi muungano kwa kutimiza wajibu na kutenda haki kama chachu ya kuhimiza maendeleo kwa watanzania.
Na Hagai Ruyagila – Kasulu
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Kamishna jenerali mstaafu wa jeshi la zimamoto na uokoaji Thobias Andengenye amewataka wananchi mkoani Kigoma kuendelea kuulinda na kuudumisha muungano ili kuleta maendeleo katika taifa la Tanzania.
Ameyasema hayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano ambayo kimkoa yamefanyika wilayani Kasulu katika uwanja wa Umoja.
Mh Andengenye amesema ni vizuri kuendelea kuulinda Muungano uliopo huku kila mmoja akitimiza wajibu wake wa kufanya kazi jambo litakalosaidia uchumi wa taifa kukua na kusonga mbele katika maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanal Isaac Mwakisu amesema Muungano huo umeleta mafanikio makubwa hapa nchini ikiwemo kuondoa ubaguzi na kuendelea kujenga mahusiano bora ya kijamii kwa pande zote mbili.
Katibu wa umoja wa wanawake mkoa wa Kigoma kupitia chama cha mapinduzi CCM Sarah Kairanya amesema chama chamapinduzi kiko tayari kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ili kudumusha Muungano uliopo.
Hata hivyo Mbunge wa jimbo la Kasulu Mjini Profesa Joyce Ndalichako amewasihi wananchi wilayani Kasulu kuendeleza amani na uzalendo wa taifa.
Maadhimisho ya sherehe za miaka 60 ya Muungano yamebebwa na kaulimbiu isemayo “Tumeshikamana na tumeimarika kwa maendeleo ya taifa letu.