Ruwasa Kigoma: Tunazalisha maji lita elfu 42 kwa siku
26 April 2024, 12:12
Wadau wa maji Manispaa ya kigoma ujiji wameomba serikali kupitia mamlaka ya maji na usafi wa mazingira kuhakikisha inafikisha maji kwa wananchi ili kuondoa adha ya kutumia maji ya isima na mito.
Na Lucas Hoha – Kigoma.
Serikali imeondoa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, baada ya kukamilisha mradi wa maji wa chanzo cha maji cha Amani Beach kilichopo kata ya Bangwe chenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 42 kwa siku huku mahitaji ya maji katika Manispaa hiyo yakiwa ni lita milioni 23 kwa siku.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira KUWASA Manispaa ya Kigoma Ujiji, Poas Kilangi wakati akitoa taarifa kuhusu utendaji kazi wa mamlaka hiyo katika manispaa ya Kigoma ujiji kwenye kikao kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa maji wakiwemo Madiwani, watendaji wa kata na wenyeviti wa mitaa.
Amesema kutokana na uzalishaji huo wa maji mamlaka imeweze kuongeza mtandao wa maji kwenye maeneo ambayo yalikuwa hayajafikiwa na huduma hiyo ikiwemo Kata za Businde na Buhanda zilizopo katika manispaa hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Salum Kalli ameipongeza serikali kwa kuendelea kuleta fedha za miradi ya maji katika manispaa ya Kigoma na kufanikisha kuondoa adha ya maji iliyokuwa inawakabili wananchi wa manispaa hiyo kwa muda mrefu.
Nao baadhi ya wadau walioshiriki kwenye kikao hicho wamesema wataendelea kutoa ushirikiano kwa mamlaka ili iweze kufanya kazi kwenye mazingira rafiki.
Hadi kufikia April 2024 mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira KUWASA imetoa huduma kwa wateja elfu 23,482 wateja walio hai kati ya hao ni ni elfu 18,713 nawateja waliositishiwa huduma ya maji ni elfu 4,770 na wateja wasiotumia mita ni 1,655.