Neema kuwashukia watoto yatima Kigoma
15 April 2024, 22:00
Jamii wilayani Kasulu mkoani Kigoma imetakiwa kutowaficha watoto wao wenye uhitaji maalum ili wapate elimu bora itakayowasaidia katika maisha yao.
Na, Hagai Luyagila
Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa maafisa elimu maalum nchini Tanzania Issa Kambi wakati wa hafla ya utoaji zawadi kutoka kwa umoja wa wadau wa watoto wenye mahitaji maalum iliyofanyika katika kituo kilichopo ndani ya shule ya msingi mwenge halmashauri ya mji Kasulu
Amesema watoto hao wanaweza kusaidiwa na ndiyo maana rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwapa kipaumbele ili waweze kupata elimu bora.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mji kasulu Vumilia Simbeye amesema halmashauri ya Mji Kasulu itaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuona umuhimu wa kuwapeleka watoto wao wenye mahitaji maalum shuleni.
Naye Kaimu afisa elimu msingi halmashauri ya Mji Kasulu Shabani Baleka amempongeza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kwa namna anavyotekeleza majukumu yake ipasavyo katika shughuli za kimaendeleo ndani ya halamshgauri hiyo.
Nao baadhi ya wazazi na walezi kutoka halmashauri hiyo wamewashukuru wadau kwa msaada walioutoa pamoja na kusisitiza kuwa wako tayari kuendelea kuwaelimisha wazazi wengine ili kuhakikisha changamoto hiyo inatokomezwa.
Baadhi ya zawadi zilizotolewa katika hafla hiyo ni Masweta 20, Kaptura 10, mashati 10, sketi 6 mchele kilo 55, mafuta lita 10, maharage kilo 20, sukari kilo 25, ngano kilo 25 na mkurugenzi wa halmashauri hiyo kutoa shilingi laki moja.