Wanafunzi wafundwa kilimo cha kahawa kibondo
15 April 2024, 12:33
Katika kukabiliana na changamoto za utegemezi kwa wanafunzi baada ya kuhitimu ngazi mbalimbali za elimu nchini kituo kidogo cha utafiti wa kahawa Tanzania TACRI ofisi za kigoma kimeanza kutoa elimu ya kilimo cha kahawa kwa wanafunzi wa sekondari Wilayani Kibondo Mkoani Kigoma.
Na James Jovin
Shule ya Sekondari Itaba iliyoko wilayani Kibondo mkoani Kigoma imefanikiwa kutatua baadhi ya changamoto mbali mbali na kuwafundisha wanafunzi elimu ya kujitegemea kupitia kilimo cha kahawa ili waweze kujitegemea kupitia kilimo.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Itaba wameeleza kunufaika na kilimo cha kahawa shuleni hapo na kwamba watahakikisha wanalima zao hilo hata baada ya kuhitimu masomo yao sambamba na kuisambaza elimu hiyo kwa wananchi wengine
Aidha wanafunzi hao akiwemo Vitus Venance na Yasinta Jeremia wamesema kuwa elimu ya kujitegemea hasa kilimo itasaidia sana wanafunzi wengi wanaomaliza shule na kukaa mitaani bila kujishughulisha na kazi yoyote.
Mkuu wa shule ya sekondari Itaba mwl Magambo Daniel amesema mradi huo wa kilimo cha kahawa ulianza mwaka 2020 shuleni hapo na kwamba umekuwa na manufaa makubwa ikiwemo kufundisha wanafunzi elimu ya kujitegemea hasa kwa wale wanaohitimu na kushindwa kuendelea na elimu ya juuu.
Meneja wa kituo kidogo cha utafiti wa kahawa Tanzania TACRI ofisi za kigoma Sophia Malinga ambaye ametembelea shule hiyo na kujionea kazi inayofanywa na wanafunzi kwa kushirikiana na walimu amesema Mwikitikio wa wananchi kwa kilimo cha Kahawa ni mkubwa huku Halmashauri ikijipanga kutafuta masoko.