Wananchi watakiwa kutokuwa sehemu ya uvunjifu wa amani Kigoma
27 March 2024, 14:49
Wakazi wa kata ya Mahembe halmashauri ya wilaya ya Kigoma wamepatiwa elimu ya namna ya kulinda amani iliyopo huku wakitakiwa kushirikiana na vyombo vya usalama katika kufichua wahalifu ambao wamekuwa chanzo cha uvunjifu wa amani.
Na, Josephine Kiravu.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo uliowakutanisha wananchi wa kata ya Mahembe pamoja na viongozi kutoka halmashauri ya wilaya ya Kigoma mgeni rasmi katika mkutano huo Bi Dora Buzaile kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Kigoma amesisitiza umuhimu wa kulinda amani ili kuepuka machafuko na kusababisha athari kwa Taifa.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliohudhuria katika mkutano huo akiwemo Ustadhi Omary Shabani wameeleza umuhimu wa amani huku wakilitaka jeshi la polisi kudhibiti vitendo vya ukatili kijijini hapo kwani vinatishia uvunjifu wa amani.
Naye mratibu wa Shirika la Search for Common Ground ambalo linajihusisha na utoaji elimu kuhusu amani Kheler Nassoro Rashid amesema wameamua kutoa elimu kuhusu amani kutokana na uwepo wa mwingiliano na nchi jirani ambazo mara kadhaa zimekuwa na machafuko huku akiitaka jamii kushirikiana kwa pamoja kulinda amani iliyopo.
Kwa mujibu wa shirika hilo la Search for Common Ground ambalo limejikita katika wilaya za Kigoma, Buhigwe na Kasulu wakiwa katika utekelezaji wa mradi wa Dumisha amani Kigoma mwitikio wa wananchi ni mzuri katika kupokea elimu licha ya baadhi kuendelea kuwa mitazamo hasi kuhusu baadhi ya matukio ikiwemo yale ya kuwakaribisha wageni ikiwemo Lambalamba ama kamchape ambao mara kadhaa wamekuwa wakisababisha uvunjifu wa amani