Wananchi wafurahia utekelezaji wa miradi ya elimu Kakonko
26 March 2024, 15:38
Wakazi wa Kata ya Kanyonza katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, wameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kujenga shule ya sekondari ya wasichana ya bweni na ambayo itatoa fursa kwa mabinti wengi kutimiza ndoto zao kielimu kwa kuepuka vikwazo walivyokuwa wakipitia.
Wakizungumza na kituo hiki baadhi wa wakazi wa kata hiyo na mwenyekiti wa kijiji cha Kanyonza ambapo shule hiyo imejengwa, wamesema shule hiyo imekuwa msaada kwa mabinti waliokuwa hatarini kutumbukia katika vishawishi na kupoteza masomo na pia kuleta nafuu kwa wazazi.
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo, wameeleza jinsi ambavyo uwepo wa shule hiyo ulivyosaidia kuepuka vishawishi ambavyo vingeweza kusababisha kutotimiza ndoto zao katika elimu.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Godfrey Kayombo, amesema serikali imewapatia fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 39.8 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo ya shule.