Wananchi Kimobwa watakiwa kuzingatia lishe bora kwa watoto
12 March 2024, 13:21
Jamii mkoani Kigoma imetakiwa kuzingatia matumizi ya vyakula vyenye lishe kwa watoto ili kusaidia kuwakinga na utapiamlo ambao unasababisha udumavu kwa watoto.
Na, Emmanuel Kamangu
Wananchi wa kata ya Kimobwa halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma wametakiwa kuendelea kuhudhuria kikamilifu siku ya lishe ya mtaa ili kupewa elimu ya makundi bora ya vyakula vinavyotakiwa kwenye lishe ya watoto.
Hayo yameelezwa na Afisa Lishe kutoka hospital ya wilaya Kasulu Bi. Rehema Stephano wakati wa siku ya lishe ya mtaa wa Kimobwa ambapo amewataka wananchi kuhakikisha wanazingatia lishe bora ili kukabiliana na udamavu pamoja na utapia mlo kwa watoto.
Kwa upande wake, afisa mtendaji kata ya Kimobwa B. Sifa Evaristo amewataka wananchi wa kata hiyo kutumia vema elimu ya lishe bora ambayo wamepewa ili kuzisaidia familia zao kuwa na afya njema.
Aidha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Koku Gonza ambaye ni mkaguzi kata ya Kimobwa amewataka wananchi kuacha tabia ya kutoa fedha kuwapa kamchape badala yake watumie fedha hizo kununua vyakula vitakavyo wasaidia kupata mlo kamili.
Wananchi ambao wameshiriki mafunzo hayo wamesema kwa kiasi kikubwa wamepata uelewa wa makundi sahihihi ya vyakula vinavyoweza kuwasaidia kuwa na afya njema.
Mafunzo hayo yametawaliwa na majiko darasa ambapo kila mwananchi amejifunza kwa vitendo jinsi ya kupika vyakula vye lishe bora.