Kigoma DC yaagizwa kuhamia kwenye ofisi zake
6 March 2024, 09:54
Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma Albert Msovela amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kigoma kuhakikisha ifikapo Julai Mosi, 2024 halmashauri hiyo inahamia katika jengo lake la Ofisi linalojengwa na Serikali katika eneo la kiutawala kata ya Mahembe wilayani humo.
Msovela ametoa maelekezo hayo akiwa katika ziara yake ya Ukaguzi wa utekelezaji Miradi ya Maendeleo mkoani hapa, ambapo amemtaka mkurugenzi huyo kuhakikisha kazi za ujenzi wa jengo hilo zinakamilika kwa haraka na ubora ili kusogeza huduma kwa Wananchi.
“hakikisha watendaji wa Ofisi yako wanahamia hapa, Serikali ya Mhe. Rais Samia Suluhu imelenga kuimarisha utoaji wa huduma bora na kuzingatia ukaribu kwa wananchi, hivyo nakuelekeza mpaka ifikapo tarehe hiyo, wakuu wa Idara na Vitengo wawe wamehamia hapa” amesisitiza Msovela.
Upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Chiriku Chilumba amesema ujenzi wa jengo hilo utakamilika mwanzoni mwa Mwezi Mei, 2024 ili ifikapo tarehe elekezwa watumishi husika waweze kuanza kutoa huduma wakiwa katika ofisi rasmi za halmashauri hiyo na kutoka katika majengo azimwa yaliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji.
“tutaongeza idadi ya mafundi sambamba na kusimamia ubora ili ujenzi huu uweze kufanyika kwa kasi ili jengo hili liweze kutumika katika kutoa huduma” amesisitiza Chiriku.