Wakuu wa mikoa kuwachukulia hatua wanaohujumu upatikanaji wa sukari
22 February 2024, 16:11
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote nchini kusimamia kwa makini usambazaji wa sukari na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote wanaohujumu upatikanaji wake.
Waziri Mchengerwa, ametoa agizo hilo Februari 21, 2024 jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa Serikali kupitia Tangazo la Serikali namba 40 lililotolewa mwezi Januari,2024 lilitoa bei elekezi na kuwataka viongozi wote wa Mikoa na Wilaya kusimamia bei elekezi iliyotolewa na Wizara ya Kilimo kwenye maeneo yao.
Ameongeza kuwa, Katika kukabiliana na upungufu wa Sukari Serikali kupitia Wizara ya Kilimo iliruhusu uagizaji wa sukari ambapo zaidi ya Tani 100,000 ziliingizwa nchini na utaratibu wa upatikanaji wa mawakala wa kusambaza sukari unaratibiwa kwenye Ofisi za Makatibu Tawala katika kila mkoa.
Ameongeza kuwa hatarajii kuona Mkuu wa Mkoa au Wilaya yeyote akishindwa kusikiliza kero za wananchi na kushindwa kutoa taarifa ya namna Serikali inavyoendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.