Watoto 61,545 kupatiwa chanjo ya surua rubella Kibondo
14 February 2024, 11:47
Watoto kuanza kupatiwa chanjo ya surua na rubela ikiwa ni mkakati wa serikali wa kuhakikisha wanadhibiti ugonjwa huo kwa watoto nchini.
Na James Jovin
Wizara ya afya imelenga kutoa chanjo ya Surua Rubella kwa watoto wapatao 61,545 wenye umri chini ya miaka mitano katika wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma wakiwemo watoto wanaoishi katika kambi ya wakimbizi Nduta.
Hatua hiyo imekuja baada ya visa vya ugonjwa wa Surua Rubella zaidi ya 103 kutokea mwishoni mwa mwaka jana katika kijiji cha Kumsenga pamoja na katika kambi ya wakimbizi Nduta
Akizungumza wakati akitoa taarifa kwa wajumbe wa kamati ya afya ya msingi kuhusu kampeni ya chanjo ya sulua afisa chanjo wa wilaya ya Kibondo bwana Malili Marugu amesema kuwa katika kambi ya wakimbizi nduta zaidi ya watoto 12,396 watachanjwa
Kwa upande wake mganga mkuu wa wilaya ya Kibondo Dr. Henry Chinyuka akizungumza katika kikao hicho amesema kuwa serikali imeamua kuanzisha kampeni ya chanjo ya ugonjwa wa surua Rubella kutokana na visa vya ugonjwa huo kujitokeza katika maeneo mengi kote nchini
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma kanali Agrey Magwaza ameitaka idara ya afya kutoa elimu ya chanjo hasa vijijini na katika kambi ya wakimbizi Nduta ili kuondoa wasi wasi kwa wananchi hasa wanaopotoshwa kuhusu chanjo ili waweze kutoa ushirikiano wa kutosha kwa lengo la kutokomeza ugonjwa wa surua Rubella.